Kamati kuu ya CCM yatangaza majina 3 ya kugombea nafasi ya uspika wa bunge la 11.
Hatimaye kamati kuu ya chama cha mapinduzi CCM imetegua kitendawili cha majina ya makada watatu watakaowania kuchaguliwa kugombea nafasi ya uspika wa bunge la 11 kupitia chama hicho kwa kuwatangaza naibu mwanasheria mkuu wa Tanzania Dk Tulia Atson, Mbunge wa Afrika Mashariki Abdula Mwinyi na naibu spika wa bunge la 10 Job Ndugai kuwa wagombea.
Katibu wa NEC itikadi na uenezi wa CCM Nape Nnauye anataja majina hayo baada ya kukamilika kwa kikao cha kamati kuu kilichokutana takribani saa moja na nusu kikitanguliwa na kikao cha kamati ya maadili kupitia majina ya makada 21 waliojitokeza kuomba nafasi hiyo.
Kwa upande wa nafasi ya naibu spika chama hicho kimesema mchakato huo utaanza mapema jumatatu November 16 kwa wanaotaka kuwania nafasi hiyo kuchukua fomu na kuzirudisha siku inayofuatia kabla ya kujadiliwa na kupitishwa majina kupitia kamati ya wabunge wa CCM huku mmoja kati ya mmoja kati ya makada aliyekuwa akiwania nafasi hiyo Banda Sonoko akipongeza mfumo unaotumika kupata nafasi hiyo.
Wakati huohuo chama cha wakulima (AFP) kimemtangaza Peter Sarungi kuwa mgombea wa nafasi hiyo huku akijinadi kama atapata ridhaa ya kuliongoza bunge atahakikisha anavunja makundi yote yanayotokana na itikadi ndani ya bunge ili bunge liwe la haki na usawa kwa wote.
Uchaguzi wa spika mpya wa bunge la 11 la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania unatarajiwa kufanyika jumanne tarehe 17 mwezi huu punde tu baada ya kufunguliwa kwake.